Sunday, November 4, 2012

MILA NA DESTURI ZA WAPARE


Wapare ni kabila kama yalivyo makabila mengine 120 nchi Tanzania na wanaishi kaskazini mwa Tanzania katika Mkoa wa kilimanjaro hasa katika wilaya za Mwanga na Same. Wilaya za Mwanga na Same ilikuwa moja ikijulikana kama wilaya ya Pare kabla ya kugawanywa na kuwa wilaya mbili yaani Same na Mwanga. wapare wamegawanyika katika sehemu mbili yaani kaskazini na kusini, upande wa kaskazini ipo wilaya ya Mwanga na Upande wa kusini ipo wilaya Same. kilugha pia wapare wamegawanyika; Wagweno wanaongea kigweno ambacho ni mchanganyiko wa Kichaga na kipare, na wapare wengine wanaongea Chasu, Kihistoria inaaminika kuwa asili ya wapare ni Kenya hasa kwenye miji ya Taveta na maeneo yote yanayouzunguka Mji huo. Neno Pare lina maana ya kuparua, kuondoa ngozi fulani au gome la mti, kwenye mti husika au kuparua samaki. Pia neno hili lina maana ya kifaa cha kuhifadhi aina fulani za vifaa kama vile visu na silaha nyingine. Kijografia Mji wa Mwanga unajihusisha sana kilimo na Mifugo. na sehemu nyingi ni milimani Milima ya Upare ni maarufu kwa ukulima wa Mahindi pamoja na mazao mengine ya chakula kama vile viazi, mihogo, Ndizi, Miwa n.k. Pia wanajihusisha na Ufugaji wa Ng'ombe mbuzi na Kondoo. Jamii ya kipare ni jamii mojawapo kati ya jamii chache za Tanzania ambazo zinatumia mfumo wa Umoja ni Nguvu na utengano ni udhaifu, yaani wanafanya kazi kwa umoja na ushirikiano wa hali ya juu ili kujiletea maendeleo yao na ya taifa kwa ujumla. Kwa kutekeleza hayo jamii hii ya kipare imejiwekea utaratibu ambao unatumika ili kujiletea maendeleo, na utaratibu huo hujulikana kama Msaragambo. watu wote hutoka na kufanya kazi ya Pamoja eidha katika shamba la ushirika au pia kutengeneza barabara, mifereji ya maji, kujenga shule, Zahanati, na mambo mabalimbali kama hayo. Jamii nyingi za kipare pia zina utaratibu wa kushirikiana hata kwa mambo madogo madogo zaidi hasa kwa familia zilizo karibu karibu zaidi, kama vile kushirikiana katika chakula, kuchota maji pia wamama wana ushirikiano hasa kwa kusaidiana katika mambo ya familia kama vile kukata kuni n.k. Na inapotokea suala sherehe au misiba pia jamii hii hupenda kutoa ushirikiano mkubwa zaidi kwa mambo yote yanayo husiana na taratibu mbalimbali za msiba kulingana na mila na desturi za ukoo husika. Kabla ya kuendelea mbele hebu tuangalie koo zilizo katika jamii hii husika ya Wapare. Kuna zaidi ya koo 25 za wapare ndani ya milima ya upare lakini hapa nitataja baadhi tu ya koo hizo, wasuya washana wasangi wasoffe wawanga walacha wankeni wambaga wagonja wanzava wavamba wamamba washamba wadee n.k. Koo hizi na nyingine ndizo zinazounda kabila hili la kipare. Kwa ujumla hawa wote wanaishi maeneo hayo ya Upareni na pia wamesambaa katika tanzania nzima. Kama yalivyo makabila mengine ya tanzania Wapare wana watani wao ambao ni wachaga ambao pia ni wenyeji wa mkoa huo wa Kilimanjaro. Wapare ni kabila lenye uvumilivu kwa mambo mbalimbali zaidi hasa. ni kabila lisilo kata tamaa haraka zaidi. Kwa leo naishia hapa na baadaye nitaweza kuchambua zaidi juu ya MILA NA DESTURI ZA KILA KOO YA KIPARE.

No comments:

Post a Comment

Tupatie maoni yako sasa!