PARE HISTORY

historia ya wapare

HISTORIA YA WAPARE


Wapare wanaishi katika miteremko ya milima ya Upare Kaskazini, iliyopo Mashariki ya Milima ya Usambaa; na Kusini Mashariki mwa mlima Kilimanjaro. Kwa mujibu wa historia kutoka katika machapisho mbalimbali, lugha inayozungumzwa na watu wa eneo hili, inajulikana kama Chasu. Wenyeji wakaitwa Vaasu, hivyo kabila hilo lilijulikana k ama kabila la Waasu. Historia inaeleza kuwa katika Karne ya 18, Waasu walikuwa wenyeji wa Kenya eneo la Taita na Taveta. Lakini, baada ya kusikia habari za maajabu ya Kilimanjaro, walifanya mikakati ya kuhama ili waishi katika mteremko wa mlima huo. Waasu walipofika karibu na maeneo ya mlima wa ajabu, yaani Kilimanjaro, walielekea sehemu za Kaskazini ili waishi karibu na Kilimanjaro, wakiwa na matumaini makubwa ya kuishi huko. Tofauti na matarajio yao, walikutana na wenyeji wa eneo hilo, Wachaga. Hata hivyo, hawakukata tamaa, waliendelea kuweka mazingira ya kujenga himaya hayo. Wachaga walipoona wanaingiliwa, waliitana na kuanza kuwafukuza huku wakipiga makelele wakisema “wapare…wapare”, ikiwa na maana wapige… wapige! Ili kuokoa maisha yao, Waasu walikimbia kuelekea sehemu za mteremko hadi eneo la Mwanga na Same, Kusini mwa mlima Kilimanjaro; na kupumzika hapo huku wakitafakari cha kufanya. Kuanzia wakati huo, Wachaga walipowaona Waasu, waliwanyooshea kidole la kusema “wapare”, jambo ambalo lilisababisha neno hilo kuwa maarufu; na ndio maana hadi leo wanaitwa Wapare, neno la Kichaga ambalo maana yake ni wapige. Simulizi za makabila, zinasema Wapare waliweka makazi ya kudumu katika eneo la Same, Kusini mwa mlima Kilimanjaro ili waweze kuangalia uzuri na maajabu ya mlima Kilimanjaro. Kama ilivyokuwa kwa makabila mengine, Wachaga na Wapare waliendelea kuwasiliana kwa njia ya utani, kwa lengo la kujenga uhusiano mwema na kudumisha amani; na hadi leo makabila hayo yanajulikana kama makabila pacha na pekee katika mkoa huo. Shughuli kubwa ya kabila hilo ni kilimo, ufugaji na uhunzi na waligawana maeneo kulingana na shughuli zao za kiuchumi. Wakati wafugaji walipenda kuishi sehemu tambarare, wakulima waliishi milimani na wafuaji wa vyuma walikaa maeneo tofauti yaliyokuwa na uwezekano wa kupata chuma. Wapare walianza kufua vyuma katika Karne ya 18. Wafua vyuma maarufu walijulikana kama Washana, ukoo ambao hivi sasa unafahamika kama Mshana. Ukoo wa Mfinanga ulijikita katika kazi ya kufua vyuma na kutengeneza vyombo mbalimbali. Ujuzi wao wa kufua vyuma, uliwasaidia kukuza uhusiano na makabila mengine hasa Wachaga na Wasambaa, ambao walilazimika kununua zana mbalimbali zinazotokana na chuma, ikiwa ni pamoja na majembe, mapanga, visu na mikuki. Kutokana na ukosefu wa vyuma, ukoo wa Mfinanga uliamua kuachana na kazi ya kufua vyuma. Lakini, katika ukoo wa Mshana hadi leo kuna baadhi ya vijana wanaendelea kuenzi kazi hiyo, kwa kutumia vyuma chakavu. Wanawake wa Kipare walikuwa mahiri kwa kufinyanga vyungu na vyombo vingine, kama birika, vikombe na sahani. Pia wanaume walikuwa mahiri kwa kuchonga vifaa mbalimbali kwa kutumia miti maalumu. Eneo la Vudee, Chome na Usangi lina udongo mzuri wa ufinyanzi, hivyo wakazi wa eneo hilo walikuwa wakitengeneza vyungu na mitungi mikubwa yenye uwezo wa kuhifadhi lita 60 hadi 100 za maji na kuiuza katika mikoa ya Tanga, Kilimanjaro na Arusha. Kwa ujumla Wapare, wake kwa waume walikuwa wamejaliwa vipaji na ujuzi katika kazi za sanaa hasa ufuaji wa vyuma, ufinyanzi na uchongaji, jambo lililoimarisha biashara na uhusiano kati yao na makabila mengine. Wapare walisifika kuwa ni wachapakazi na watu wenye vipaji vya kipekee, hivyo walijipatia umaarufu na hatimaye wakaweza kuwa na ushawishi mkubwa katika masuala ya kiuchumi na kisiasa. Ingawa Wapare wanategemea kilimo, hali ya ukame imesababisha wajikite katika elimu ili kuweza kupata kazi sehemu mbalimbali, jambo linalowawezesha pia kukabiliana na changamoto zinazosababishwa na utandawazi. Ingawa hakuna takwimu rasmi, zinazoonesha jinsi Wapare walivyojikita katika elimu, inaaminika kuwa Wapare ni miongoni mwa makabila machache, ambayo watu wake wamewekeza katika elimu na wana ushawishi mkubwa wa kisiasa na kiuchumi katika Taifa la Tanzania. Wapare ni miongoni mwa makabila yanayopenda haki. Hawapendi kuonewa wala kumuonea mtu. Wanapokutana na hali ya uonevu, hukimbilia kwenye vyombo vya kusimamia sheria, kitendo kinachojenga dhana kuwa ‘wanapenda kesi’. Ingawa baadhi ya mila na desturi ya makabila mengi zilipuuzwa, Wapare wamekuwa na sifa ya kukataa dhuluma, hivyo matambiko yalikuwa na kipengele cha kukataa dhuluma. Kabla ya kuenea kwa dini, Wapare walikuwa na sala tofauti kwa kila koo. Eneo lao la tambiko, linaitwa ‘mshitu.’ Matambiko hayo yalifanyika katika milima ya Upare, ambayo inaaminika kuwa makazi ya miungu ya Wapare. Imani hiyo iliwawezesha Wapare kuheshimu milima hiyo na kuitunza misitu iliyopo. Wapare wa Kaskazini maeneo ya Usangi, walifanya matambiko yao katika misitu ya Kindoroko, wakati Wapare wa kusini walitumia misitu ya Shengena. Hata hivyo, matambiko na dini za asili zilitoweka baada ya kuenea kwa dini za Kiislamu na Kikristo kati ya Karne ya 19 na 20, jambo ambalo pia limesababisha uharibifu wa mazingira katika milima ya Upare. Kabla ya uhuru, Wapare walikuwa na utawala wa kichifu maarufu kama Mfumwa. Machifu maarufu walikuwa chifu wa Ugweno na Chifu wa Usangi kwa upande wa Kaskazini; na Mbaga kwa upande wa kusini. Hata hivyo, utawala huo ulitoweka baada ya Tanganyika kupata uhuru mwaka 1961, kutokana na Rais wa awamu ya kwanza, Mwalimu Julius Nyerere, kupiga marufuku utawala wa Kichifu, kwa lengo la kuimarisha umoja na mshikamano kwa kuheshimu serikali moja. Kabla ya kuenea kwa elimu kutoka nchi za Magharibi, Wapare walikuwa wanatumia mbinu za kijadi, kutoa elimu kwa watoto wao ili waweze kukua katika maadili mema. Tofauti na maisha ya sasa, ambapo ndoto ya baadhi ya wazazi ni kutafuta fedha, mali na vyeti vya mfanyakazi bora, miaka iliyopita kila Mpare alikuwa na ndoto ya kuwa mzazi au mlezi bora na walitenga muda wa kutosha kukaa na watoto wao na kuwafundisha maadili mema ili waweze kurithi na kuendeleza mali za familia. Wapare wana desturi na mafundisho imara ya kimila, yanayojulikana kama Maluthumo. Mafundisho hayo yanayojumuisha methali, simulizi na mifano mbalimbali, yanatumika kutoa mwongozo kwa watoto wadogo ili kuwawezesha kufuata kanuni za maisha katika familia na kuzingatia utamaduni wa Wapare. Mambo makuu katika mafundisho hayo ni jinsi ya kuwaheshimu wazazi na kwamba kila mzee anapaswa kuheshimiwa. Endapo mtoto atakaidi mafunzo hayo, inaaminika kuwa atapatwa na laana na maisha yake yatakuwa mabaya, kwa sababu atakuwa na balaa na mikosi, kwa kukosa baraka za wazazi. Mtoto anapofikia umri wa kubalehe, anapanda daraja na kupewa mafunzo ya ujana, ambapo wasichana na wavulana hutengwa wakati wa kutoa mafunzo hayo. Wakati wavulana hupewa mafunzo, yanayojulikana kama ‘ngathu ya mshitu’. Wasichana hupewa mafunzo yanayojulikana kama ‘kieko’. Bila kujali tofauti zao kijinsia, Wapare hutoa mafunzo ya uraia ili kuwawezesha vijana kutambua thamani ya Utaifa wao. Pia, kila kundi kufundishwa jinsi ya kuishi na kutunza familia, ikiwa ni pamoja na kujenga ujasiri, busara, kutunza siri na mbinu za kuhimili changamoto zinazojitokeza katika maisha. Hata hivyo, utamaduni kupeleka vijana wa kiume jando (mshitu) ambako hupewa mafunzo jinsi ya kuishi na familia umeanza kutoweka kwa sababu asilimia kubwa ya vijana wa Kipare, wanapata mafunzo shuleni. Utaratibu wa kupeleka vijana jandoni, hufanywa na watu wachache. Kwa mujibu wa mila na desturi za Wapare, msichana anapofikia umri wa kuolewa huongeza uhusiano kati yake na mama mzazi, shangazi na dada zake ili aweze kupata ushirikiano na baraka kwa mtoto, atakapojaliwa kupata mtoto. Binti wa Kipare anapojifungua, hupaswa kupewa baraka inayojulikana kama ‘Mchumbi’ au ‘Kitonga’ kwa Wapare wa Kaskazini. Tukio hilo hupewa heshima sawa na ubatizo kwa upande wa Wakristo, na hufanyika ndani ya miezi miwili mara mtoto anapozaliwa. Wahusika huandaa sherehe, kwa lengo la kumbariki mtoto na kumpongeza mwanamke aliyejifungua. Katika sherehe hiyo, wahusika huvaa nguo nzuri za heshima na wakati wa sherehe huimba nyimbo za furaha, wakiwa na wamebeba vikapu vikubwa kichwani. Ndani ya vikapu hivyo, huweka zawadi za asili ikiwamo kuku, asali, maziwa, ndizi zilizokaushwa zinazojulikana kama ‘makafi’, nguo za mtoto na khanga za mama. Familia zenye uwezo, hupeleka mbuzi. Utamaduni huo unaendelea hadi leo, ila hutoa zawadi za kisasa, ikiwa ni pamoja na sabuni, mafuta ya kupikia, unga wa sembe, sukari na zawadi nyingine za kisasa. Kabla ya kuingia kwa dini ya Kiislamu na Kikristo, Wapare walikuwa wanatoa majina ya watoto kulingana na matukio, eneo au kwa kuzingatia siku mtoto alipozaliwa, kama vile Sengondo kwa mtoto wa kiume na Nangondo, kwa mtoto ya kike majina ambayo yanatolewa kwa watoto waliyozaliwa wakati wa vita, ambayo kwa Kipare huitwa ‘ngondo’. Ingawa siku hizi, Wapare wameshika dini ya Kiislamu na Kikristo, bado wameshikilia imani ya asili kwamba upo uhusiano kati ya wafu na waliyo hai. Kwamba wafu wakiwa na furaha, basi waliohai watapata neema na kuishi kwa furaha. Ila wafu wakikasirika, waliohai wataandamwa na balaa na mikosi, ikiwa ni pamoja na ajali, magonjwa na mikasa ambayo vyanzo vyake vinatatanisha. Ili kuondokana na balaa na mikosi, watu walio hai hulazimika kuwatuliza wazee wa zamani kwa kuwapatia nyama, pombe au maziwa. Ingawa Wapare wa kipindi hiki, hawazingatii taratibu na matambiko ya asili, bado wanathamini maeneo ambayo yalitumika kuzika watu wa kale ambayo yalitumika pia kufanyia matambiko na ibada. Ili kulinda makazi ya wazee wa kale, Wapare wa Kusini hutumia majina ya ukoo kutambulisha eneo. Kwa mfano, eneo la ukoo wa Mchome linajulikana kama Chome, eneo la ukoo wa Mbwambo linaitwa Bwambo na eneo la ukoo wa Mgonja linaitwa Gonga. Eneo la Mbaga huishi ukoo wa Mbaga, na Ndeme huishi ukoo wa Mndeme. Wapare wanaogopa laana. Hivyo hujitahidi kufanya kila liwezekanalo, kujiepusha na laana. Laana huweza kumpata mtu, endapo atadharau wazazi wake, wazee wa ukoo wake au kupuuzia mila na desturi hasa kudharau wazee wa kale. Kwa Wapare, bahati hujulikana kama ‘Lute’ hivyo bahati mbaya au laana huitwa ‘Lute luvivi’ na bahati nzuri au baraka huitwa ‘Lute lwedi’. Hivyo kila mtoto na kijana wa Kipare, hupaswa kuzingatia mafundisho ya wazazi, mila na desturi ili kupata baraka. Kama ilivyo kwa Wachaga, Wapare hasa wa Mwanga, wamegawanyika sehemu mbili yaani Wasangi na Wagweno; na wanaweza kutambulika kutokana na lahaja na maeneo wanayoishi. Wakati Wasangi wanazungumza kwa kutumia lahaja ya Waasu, wanaoishi maeneo mengine, inadaiwa kuwa lahaja ya Wagweno ni mchanganyiko wa lugha ya Waasu na Wachaga. Ingawa Wachaga ndio watani pekee wa Wapare. Lakini, kabila hilo lina uhusiano mzuri na makabila ya Mkoa wa Tanga, hasa Wasambaa, Wazigua na Wanguu.


6 comments:

  1. Masahihisho:Ni Senkondo badala ya Sengondo, Nkondo au Nankondo badala ya Ngondo au Nangondo.

    ReplyDelete
    Replies
    1. Jina Sengondo ni wapare wa mwanga wanalitumia, huku senkondo wakitumia wapare wa same

      Delete
  2. ni ipi asili ya ukoo wa wachomvu

    ReplyDelete
  3. Article hii ni nzuri sanaa
    Inafaa hata kitaaluma pongezi zimfikie muandaaji.
    Na ni vizuri tukifanya mpango wa dictionary maana lugha yetu ni mioongoni mwa lugha ambazo hazijaandikwa kwa matumizi ya badae.
    Asnte by Mngalle

    ReplyDelete
  4. Kiongozi wa wapare alikuwa anaitwa nani?

    ReplyDelete
  5. Natamani kujua maana ya jina mkodo katika lugha ya kipare ni nini na je kuna ukoo wa mkodo au ni majina tu

    ReplyDelete

Tupatie maoni yako sasa!